Jumatano, 5 Mei 2021

CHAMBILECHO FIDEL CASTRO, "MHUKUMUNI MWL BASHIRU, HISTORIA ITAMWACHIA HURU."

CHAMBILECHO FIDEL CASTRO, "MHUKUMUNI MWL BASHIRU, HISTORIA ITAMWACHIA HURU."

Na Sabatho Nyamsenda 

Leo nimeamka nikitafakari kuhusu mwalimu wangu Dk. Bashiru Ally. Tafakuri imenipeleka mbali hadi mwaka 2011, nikiwa mwaka wa tatu wa shahada yangu ya kwanza pale UDSM. Nyakati hizo nilikuwa mwenyekiti wa chama cha wanafunzi kilichojulikana kama Sauti ya Vijana Tanzania (SAVITA), huku Mwalimu Bashiru akiwa ndiye mlezi wetu. Mwaka huo, nilishiriki kuhariri jarida la Kigoda cha Taaluma cha Mwl Nyerere lililokuwa na lengo la kuadhimisha miaka mitatu ya "Kigoda", chini ya Prof Issa Shivji. 

Mimi na mhariri mwenzangu tulikusanya makala kutoka kwa Wana-Kigoda zinazohusu ya tafakuri zao juu ya shughuli za kitaaluma na kimapambano zilizoongozwa na Kigoda. Mchangiaji mmoja hakutuma makala bali shairi. Shairi liliitwa, "Heko Nyingi Nawapeni, Kwa Kutimiza Ahadi." Mchangiaji huyo ni Dk Bashiru Ally, enzi hizo tukimwita "Mwalimu Bashiru." Na alilighani shairi hilo katika Tamasha la Kitaaluma la Mwalimu Nyerere mwezi Aprili 2011.

Mwezi Mei 2011 SAVITA iliandaa Kongamano la Kuadhimisha miaka 44 ya Azimio la Arusha. Mtoa mada alikuwa ni Prof Shivji, na mwongozaji ni Mwl Bashiru. Baada ya kongamano hilo nilistaafu uenyekiti wa SAVITA. Katika hotuba yangu ya kukabidhi uongozi, niliandika maneno haya, huku nikinukuu baadhi ya beti kutoka kwenye shairi la Dk Bashiru nililolitaja mwanzoni:
________________________
"Kwa walioishika vema, SAVITA iligeuka kuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku. Matendo yao, mazungumzo yao, mavazi yao, matarajio yao, mitazamo yao na hata maamuzi juu ya nani awe rafiki ama adui vilijengeka katika misingi ya SAVITA  niliyokwishaitaja hapo awali. Lakini, ashakum si matusi. Tuna jamii ya ajabu. Katika zama hizi za utandawazi, kuishika misingi hiyo ni ‘uendawazimu’. Tuna jamii ambayo itakushangaa usipoiba, itakukujeli usiposema uongo na itakutukana ukijidai una moyo wa kujitolea. Mwalimu Bashiru Ally aliyaona hili, ndio maana akaghani:

"Vita mliyoasisi, ni vita ya ukombozi,
Kukomboa Almasi, na samaki wa Zambezi,
Vilevile kuziasi, sera za ‘utandawizi’,
Heko nyingi nawapeni, kwa kutimiza ahadi.

"Vita ikishakolea, mtaiwa magaidi,
Hongo msipopokea, mtaitwa wakaidi,
Ushindi ukiwadia, mtaitwa mashahidi,
Heko nyingi nawapeni, kwa kutimiza ahadi."
___________________________

Miaka 10 imepita tangu niitoe hotuba ile. Sikujua kuwa niliyokuwa nikiyasema ndiyo yatamkuta gwiji huyu wa mapambano. Na shairi la Dk Bashiru pia limetimiza miaka 10. Nafikiri wakati akiliandika na kulighani hakuwa amejua yatakayotokea leo. 

Kosa pekee alilofanya ni kuokoa mali za chama chake, ambapo hapo awali zilisemekana kuwa na thamani ya bilioni 60, ila baada ya uhakiki wa Kamati aliyoingoza ikagundulika kuwa zina thamani ya trilioni 1 (kwa mujibu wa vyombo vya habari). Mali za zaidi ya bilioni 940 zilikuwa zimeporwa na walafi, huku chama chake kikiwa kimewekwa mfukoni mwa mafisadi. Hao ndio wanaoongoza kumchafua leo hii. 

Mara baada ya kuteuliwa kuwa katibu mkuu wa CCM, ziara yake ya kwanza aliifanya katika ofisi za Mtandao wa Wakulima Wadogo Tanzania - MVIWATA. Haikuwa mara ya kwanza kufika hapo bali alikuwa ni rafiki wa MVIWATA kwa muda mrefu kabla ya kuteuliwa. Hiyo ilifungua mlango mpya wa mshikamano katika kupambana dhidi ya uporaji wa ardhi, mbegu za kifo za GMO, rasimu ya sera mpya ya kiporaji ya ardhi, nk. Vijiji vya Msowero (Kilosa), Lukonde na Mtego wa Simba (Morogoro Vijijini), Mchukwi (Kibiti), Amboni (Tanga), na kwingineko vinamkumbuka kwa jinsi alivyoungana nao kupambana na mtandao wa waporaji wa ardhi, waliokuwa wakichoma nyumba za wanavijiji, kuwapiga na kuwafungulia wanavijiji mashtaka ya kughushi na kuchoma mazao yao mashambani. Haya huwezi kuyasikia kwenye vyombo vya habari. Kwa wavujajasho hao waliporwa ardhi, Mwalimu Bashiru ni shujaa. Huko wanamwombea dua na kumtakia heri. Ni nani atakayesikia sauti zao?

Mwaka jana, nikizungumza na Fr. Privatus Karugendo, aliniambia kuwa alishangazwa sana alipofika nyumbani kwa Bashiru akiwa katibu mkuu wa CCM. "Nyumba iko tupu. Anaishi maisha very simple," Fr Karugendo alinambia, huku akifurahi kuwa cheo hakikum-badilisha Bashiru. Hata alipolazimika kuvaa suti katika dhifa za kitaifa, alivaa 'suti za Kaunda' na sio koti na tai. Lakini vyake ni viatu vya wazi (sandles), suruali na shati.  
 
Bashiru sio mtu wa vyeo na wala hakugombea cheo chochote. Aliteuliwa. Huyu ni mjamaa na wanamajumui wa Afrika. Samaki kwake majini, mjamaa kwake mapambanoni. Mwalimu wake, Nyerere, alipotoka Ikulu alirudi Butiama kushika jembe na kucheza bao na wanavijiji. 

Natumai Mwl Bashiru atakapomaliza kutumikia nafasi yake ya uteuzi ya sasa, atarudi chuoni kufundisha, kutafiti na kushiriki katika mapambano ya wavujajasho kudai haki zao. Natumai tutapanda wote basi kwenda Morogoro kwenye mikutano ya MVIWATA. Natumai tutapanda tena bodaboda kwenda vijijini kujifunza kwa wavujajasho. Natumai atatutungia na kutughania mashairi ya kimapinduzi. Natumai tutakusanya tena maandiko ya wanamapinduzi, kuyatafsiri na kuyachapisha.

Fidel Castro alipotiwa korokoroni kwa kupambana dhidi ya ujahili nchini Cuba, alisema, "Nihukumuni. Historia itaniachia huru." Naam, historia ya mapambano dhidi ya ufisadi na uporaji wa rasilimali za wavujajasho itamwachia Mwl Bashiru huru. Na historia hiyo haitaandikwa na walafi na mafedhuli aliopambana nao. Itaandikwa na wakulima wadogo, wamachinga na bodaboda.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Historia ya Grand P

Grand P Msanii Mwenye Mvuto wa Aina Yake  Thread starte Jina la kuzaliwa:   Moussa Sanguiana Kaba  Mwaka wa kuzaliwa: 1990 Umri: Miaka 31(mw...